Homo ergaster alionekana barani Afrika takribani miaka milioni 2 iliyopita . Mara nyingi huchukuliwa kuwa spishi ya kwanza ya kweli ya binadamu. Tayari alikuwa na mwili wa kisasa, ubongo mkubwa zaidi, aliweza kutembea wima kwa ufanisi, na alionyesha maendeleo muhimu katika fikra na tabia za kijamii. Inadhaniwa kuwa spishi hii iliibuka kutokana na mabadiliko makubwa ya mazingira, hasa kuenea kwa savana kavu na wazi katika Afrika Mashariki.
Acheulian inaonyesha mabadiliko haya ya kibaolojia na kimazingira. Imepewa jina kutoka kwenye eneo la nchi ya Ufaransa la Saint-Acheul, ambapo iligunduliwa kwa mara ya kwanza karne ya 19, teknolojia ya acheulian iliwezesha binadamu kutengeneza vipande vikubwa vya jiwe (urefu zaidi ya sentimita 10) kutoka kwenye jiwe kubwa zaidi litumikalo kama chanzo cha mawe mengine. Pia waliweza kutengeneza zana kubwa za kukata, kama vile shoka la mkononi, zana za mawe zifananazo na sururu, mawe makubwa ya kukatia, na visu. Ubunifu huu uliwakilisha hatua kubwa mbele katika mageuzi ya binadamu.
Makundi haya pia yalianza kupanga na kutumia mandhari kwa njia mpya. Walikuwa na maeneo makubwa ya makazi na mifumo ya kijiografia yenye ugumu zaidi. Ukuaji wa ujuzi wa fikra na kijamii unaonekana wazi katika utengenezaji wa zana kubwa za mawe zilizopangwa kwa viwango vinavyofanana na usambazaji wake wa kijamii. Aina mbalimbali za zana pia zinaonyesha lishe tofauti zaidi na njia mpya za kupata na kuchakata chakula.
Ushahidi wa awali wa Acheulian barani Afrika unarudi karibu miaka milioni 1.9 hadi milioni 1.7 iliyopita. Maeneo muhimu ya awali ni Kokiselei 4 nchini Kenya, Melka Kunture na Konso nchini Ethiopia, pamoja na FLK Magharibi nchini Tanzania. Maeneo ya baadaye, kutoka miaka milioni 1.5 hadi milioni 1.2 iliyopita, yamepatikana sehemu mbalimbali za Afrika, ikiwemo Bonde la Oldupai na Pinyinyi nchini Tanzania.
Timu yetu imekuwa ikichunguza Acheulian nchini Tanzania kwa miaka mingi. Kwenye tovuti hii, unaweza kuchunguza utafiti wetu unaoendelea katika FLK magharibi (Bonde la Oldupai) na Pinyinyi (Ziwa Natron), pamoja na miradi mingine, data, na taarifa mpya kuhusu Acheulian barani Afrika. Karibu sana!






























